https://monetag.com/?ref_id=TTIb Dodoma kupambana na vifo vya wakina Mama na Watoto | Muungwana BLOG

Dodoma kupambana na vifo vya wakina Mama na Watoto



Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge amezindua rasmi kampeni ya ‘JIONGEZE! TUWAVUSHE SALAMA’ jijini Dodoma, kampeni ambayo imelenga kumsaidia mama mjamzito kujifungua salama.Katika hotuba yake Mhe.Mahenge, amewataka viongozi wote kuwa washiriki na watendaji wa kampeni hii, ili kuhakikisha mama anakuwa salama kwa kutoa elimu ya uzazi popote kwa wananchi.

Aidha, amesema lengo la tamko hili ni kuongeza kasi ya uwajibikaji katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga nchi nzima.

"Tumeamua kuchukua kuchukua hatua hii muhimu kwa sababu, kifo cha mama mjamzito au anayejifungua au aliyejifungua na kifo cha mtoto mchanga aliyezaliwa havikubaliki,’’ alisema Dkt. Mahenge.

Hata hivyo, amezitaja sababu kuu zinazosababisha vifo hivi kwa kina mama kuwa ni pamoja na kutokwa na damu nyingi kabla na baada ya kujifungua, kifafa cha mimba, kuchanika kizazi, upungufu mkubwa wa damu, kondo la nyuma kushindwa kutoka, matatizo yatokanayo na ugonjwa wa UKIMWI, uchungu pingamizi, matumizi ya dawa za miti shamba zinazoaminika kuongeza uchungu wa kujifungua na matatizo yatokanayo na kuharibika kwa mimba kwa njia yoyote ile.

Dkt. Mahenge amesema kuwa sababu za vifo vya watoto wachanga ni pamoja na kushindwa kupumua kwa mtoto akiwa tumboni na mara baada ya mama kujifungua, matatizo yatokanayo na kuzaliwa njiti na matatizo ya ulemavu wa kuzaliwa nao (Congenital abnormalities).

Mkuu wa Mkoa huyo amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa Tanzania kwa mwaka 2017, vifo vya wanawake wajawazito 556 kwa kila vizazi hai 100,000 vilitokea, na lengo la Serikali ni kupunguza vifo hivi hadi kufikia 292 kwa vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2020.

Ameongeza kuwa kwa mwaka 2017, vifo vya watoto wachanga ni 25 kwa kila vizazi hai 1,000 na lengo ni kupunguza hadi kufikia vifo 16 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2020.