https://monetag.com/?ref_id=TTIb Dodoma ni shwari, tuko tayari kuupokea ujio wa Rais - Askofu Mallasy | Muungwana BLOG

Dodoma ni shwari, tuko tayari kuupokea ujio wa Rais - Askofu Mallasy


Askofu wa Kanisa la Tanzania Fellowship of Churches (TFC), Dk. Godfrey Mallasy amesema Jiji la Dodoma kwa sasa ni shwari na liko tayari kwa ujio wa Rais, Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumapili, Februari 11, 2019) wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kanisa la Dodoma Christian Centre mara baada ya kumaliza ibada maalumu ya kuombea ujio wa Rais Magufuli jijini Dodoma.

Askofu Mallasy alikuwa akihitimisha semina ya siku nne ya jinsi ya kutambua madhabahu zinazokutesa na kuzivunja na kisha kufunguliwa.

Alisema TFC iliandaa semina hiyo kwa kushirikiana na makanisa mengine na kuamua kuhitimisha kwa maombi ya kuvunja madhabahu za mkoa wa Dodoma na kujenga madhababu ya kitaifa.

“Ndoto ya Serikali kuhamia Dodoma inakaribia kutimia kwa sababu wizara zote zimeshahamia hapa na Mheshimiwa Rais wetu anakaribia kuhamia. Kwa hiyo, viongozi wa kiroho tunao wajibu wa kumuandalia makazi yake ya kiroho. Jambo lolote likitokea, basi ujue limeanzia rohoni,” alisema.

“Leo tuko Dodoma, madhabahu ya hapa inasema kila kitu kitadidimia (kutokana na asili ya neno Dodoma – idodomya- linalomaanisha kudidimia). Na falme za hapa zimetamka hilo lakini baada ya maombi haya, sisi tunasema Dodoma haitadidimia, bali itaamka.”

Alisema maneno hayo kupinga hali ya uduni wa Dodoma, yanaendana na ujasiri wa Serikali ya awamu ya tano kuhamishia shughuli zake zifanyike makao makuu ya nchi, Dodoma.

Mkesha wa kuliombea Taifa, umekuwa ukifanyika nchini kila mwaka kuanzia mwaka 1997.