Fedha za maboresho shule kongwe zitumike kwa lengo lililokusudiwa - Dkt. Kijaji


Serikali imewataka watendaji katika maeneo yote ambayo fedha zimetolewa zikiwemo sh. bilioni 18 za kuboresha shule kongwe nchini, kusimamia matumizi yake ipasavyo ili kufikia lengo lililokusudiwa na kwa ubora unaotakiwa.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, alipotembelea na kukagua maboresho ya Shule Kongwe ya Sekondari ya Wasichana Korogwe, Mkoani Tanga, ambayo hivi sasa imekuwa ya kisasa na mwonekano mzuri.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali imeamua kutekeleza kazi zake nyingi kwa mfumo ujulikanao kama Force Account, ambao unatoa fursa kwa Wakandarasi wazawa kushiriki kikamilifu kwa lengo la kufanikisha maendeleo kwa gharama nafuu na kwa ubora unaotakiwa.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe, Bi. Annisia Mauka, katika taarifa ya utekelezaji wa maboresho ya shule hiyo, alisema,   Serikali, kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) iliwapatia kiasi cha  Sh. bilioni1.3 kwa ajili ya kujenga miundombinu 27 ya Shule, ikiwemo umeme, majisafi na taka na pia Mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

"Tumefanikiwa kukarabati majengo 26 ambayo ni pamoja na  vyumba vya madarasa 23,  maabara, maktaba, jengo la utawala, mabweni, bwalo la chakula, vyoo vyenye matundu 116, jengo la Zahanati, Mfumo wa Maji taka na safi na pia mfumo wa kupikia kwa njia ya nishati ya gesi," alifafanua Bi. Mauka.

Alisema kuwa hadi sasa fedha zilizotumika kununulia vifaa ni takribani Sh. bilioni 1.05 huku gharama za ufundi zikiwa Sh. milioni 315.9 hivyo kusalia na zaidi ya Sh. milioni 2.09.

Bi. Mauka, ameiomba Serikali kufanikisha ujenzi wa Bweni jipya linalogharimu zaidi ya Sh. milioni 109.6 kwa kuwa Bweni hilo lilishindikana kufanyiwa maboresho kwa kuwa uharibifu wake ulikua mkubwa baada ya kufanyiwa tathmini ya kina, pia aliiomba Serikali kufanikisha ujenzi wa ukuta wa Shule hiyo kwa kuwa kukosekana kwa ukuta huo kunahatarisha usalama wa wanafunzi na watumishi wengine.

Naibu Waziri Dkt. Kijaji, ameahidi kufanyia kazi maombi hayo kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mhe. Mary Chatanda, na kutoa agizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, kufanya tathmini ya gharama ya ukuta huo ili kujua gharama halisi  kwa lengo la kupata fedha za ujenzi ili kulinda usalama wa Wanafunzi.