Jafo alipongeza Jiji la Dodoma kwa kukusanya Bilioni 40


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo ameipongeza Halmashauri ya jiji la Dodoma kwa kuweza kukusanya zaidi ya Sh.Bilioni 40 ndani ya miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba mwaka 2018.

Pamoja na pongezi hizo, ameitaka Kamati ya fedha na utawala ya jiji hilo kuhakikisha inasimamia matumizi bora ya mapato hayo.

Jafo ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akifungua mafunzo kwa kamati ya fedha na utawala pamoja na Kamati ya ukaguzi za jiji la Dodoma yaliyoandaliwa na Taasisi ya WAJIBU kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani(GIZ) kupitia mradi wa usimamizi bora wa fedha za umma.

Amesema makusanyo yaliyokusanywa na jiji la Dodoma ni sawa na makusanyo ya Halmashauri 20 hivyo inatakiwa kufanya vizuri kwenye matumizi yake na kujibu matatizo ya wananchi.

"Sh.Bilioni 40 sio fedha ndogo kuna halmashauri pato lake la mwaka mzima wanakusanya Sh.Bilioni 2, mnafanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato kuna wengine wanasema yanatokana na viwanja mbona halmashauri zingine zinauza na hazifikii makusanyo hayo,"amesema.

Ameeleza kuwa jiji hilo ndo jiji pekee lililoweza kufikia kiwango hicho.

"Mnafanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato na ninyi mnatakiwa muendelee kufanya vizuri, sasa kazi mliyonayo ni jinsi gani mtahakikisha mnabaki kwenye nafasi hiyo,"alisema.

Amebainisha kuwa pamoja na kufanya vizuri kwenye mapato wahakikishe matumizi yao yanafanyika vyema kwa kuwa miongoni mwa hoja za ukaguzi zilizopo kwenye halmashauri nchini ni kutozingatia matumizi bora.

"Nataka jiji hili liwe la mfano kufundisha majiji mengine na ifikie uwezo wa kujitegemea na kuwa na fedha za ziada, nimeona mikakati yenu kuna soko kubwa halijawahi kutokea nchini linajengwa hili litaipasisha sana kimapato halmashauri hii pamoja na kituo cha mabasi kinachojengwa,"amesema.

Amewataka viongozi wa halmashauri hiyo ikiwemo madiwani kuacha majungu yatakayosababisha utendaji kazi kukwama.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya WAJIBU Ludovick Utouh alisema mafunzo hayo yanalenga kuzijengea uwezo kamati hizo katika masuala ya ukusanyaji na usimamizi bora wa rasilimali za umma.