.

2/11/2019

Jenerali Mabeyo awasili Njombe sakata la Mauaji ya Watoto


 Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania CDF, Jenerali Venance Mabeyo amewasili mkoani Njombe kwa ajili ya kuona mwenendo wa matukio ya utekaji na mauaji ya watoto na hatua zilizofikiwa katika oparesheni zinazochukuliwa na vikosi kasi maalumu vilivyotumwa kutafuta kiini cha matukio hayo.

Akizungumza mara baada ya kuwasuli mkoani humo amesema kuwa matukio hayo ni ya kifamilia zaidi, hivyo watayashughulikia kwa upande huo zaidi.

"Pasiwepo na hofu kwamba suala hili limekuwa la kitaifa zaidi, hapana. Suala hili pengine linahusu familia moja moja, ni la kifamilia zaidi, sasa kama ni ya kifamilia lazima itafute njia ya kuyadhibiti ili yasiendelee kutokea kwa wengine," amesema Jenerali Mabeyo.

Hivi karibuni Bungeni Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola alitoa tamko la serikali kuhusu
mauaji ya watoto yanayoendelea mkoani humo.

Alisema kuwa tayari watu 29 wanashikiliwa na jeshi hilo na tayari timu ya wapelelezi imetumwa mkoani humo kuvisaidia vyombo vya dola kuchunguza matukio hayo kwa kutumia falsafa ya ulinzi shirikishi.