Jeshi la Polisi lafanikiwa kuwakamata watuhumiwa 30 matukio ya mauaji Njombe


Jeshi la Polisi Makao Makuu  Kitengo Maalum cha Kupambana na uhalifu kikiongozwa na Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi Naibu Kamishna Liberatus Sabas, kimeshirikina na Jeshi  la  Polisi Mkoa wa Njombe  kuendesha Operesheni  Maalum  ya kukabiliana na matukio ya mauaji ya watoto wadogo ambayo yamejitokeza mkoani humo, mpaka sasa watuhumiwa 30 wamekamatwa waliojihusisha na matukio hayo.

Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi Naibu Kamishna Liberatus Sabas, amesema watuhumiwa hao ifikapo Jumatatu watakuwa wamefikishwa Mahakamani kukabiliana na tuhuma  za mauaji ya watoto.

 Aidha Naibu Kamishna Sabas, amewataka  Watanzania kutoa taarifa za wahalifu  popote walipo na amewahakikishia Watanzania kuwa matukio hayo yamekoma sasa.

Hata hivyo, Naibu kamishna Sabas amesema  Jeshi La Polisi halitamuonea mtu yoyote haya awe Mfanyabishara, Viongozi wa Serikali, Viongozi wa Dini, au Waganga wa Kienyeji watakaojihusisha na matukio ya mauaji kwa njia yoyote ile sheria itachukua mkondo wake huku akiapa kupambana na wahalifu wa mauaji yoyote yale kindakindaki.