Kusambaratika kwa siasa za dunia Merkel aonya


Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amotoa onyo kali dhidi ya kuuachia muundo wa siasa za dunia kusambaratika, na kutoa mwito ya kuinusuru mikataba ya kimataifa ambayo Marekani imeipa kisogo.

Akihutubia mkutano wa kimataifa kuhusu usalama unaofanyika mjini Munich, Bi Merkel amesema ''hatuwezi kuiacha (mikataba hiyo) ivunjike na kusambaratika'' kwa sababu ipo mizozo mingi inayoikabili dunia.

Kauli ya Kansela Merkel ambaye atastaafu baada ya muhula wake kumalizika mwaka 2021, imechukuliwa kama karipio kwa hatua za Rais wa Marekani Donald Trump. Hotuba yake ndefu imeonekana kama kilele cha mkutano huo uliohudhuriwa na wakuu wa nchi na wa serikali wapatao 30, na imeshangiliwa sana na washiriki.

Merkel ameuangazia mkataba kati ya Urusi na Marekani kuhusu makombora ya nyuklia ya masafa ya kati (INF) ambao Marekani imesema itajiondoa rasmi mwezi August, akisema hatua hiyo ya Marekani ilikuwa ''haiepukiki''. Marekani imeishutumu Urusi kukiuka mkataba huo, shutuma ambazo Urusi imekuwa ikizikanusha.

Kansela huyo wa Ujerumani ametaka China ijiunge katika mazungumzo yatakayoweka mkataba mpana zaidi katika misingi ya INF, akisema kudhibiti mashindano ya kutengeneza silaha za maangamizi ni suala lililoihusu kila nchi.