.

2/11/2019

Mahindi yaanza kusafirishwa na NFRA


Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umeanza kusafirisha mahindi kwenda nchi zenye njaa tani 36,000 ikiwa ni sehemu ya mkataba baina yake na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP).

Hayo yamebainishwa jana na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Vumilia Zikankumba, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu usafirishaji huo.

Zikankumba alisema kuwa wameshasafirisha mahindi takribani tani 15,000 kwenda katika Uganda na Sudani Kusini.

Alisema mkataba huo ambao uliingiwa kati ya NFRA na WFP ambao pia ulishuhudiwa na Rais John Magufuli, na katika awamu ya kwanza ya mkataba watasafirisha tani 36,000.

"Tumeshasafirisha nusu ya mkataba wetu unaotutaka kusafirisha mahindi tani 36,000, ambapo hadi hivi sasa kama mnavyoona hapa shughuli zinaendelea na tumesafirisha nusu ya mkataba ambapo tani 15,000 zishakwenda nje ya nchi," alisema Zikankumba.

Aidha, aliwataka wakulima kutumia fursa hiyo ya NFRA, kuuza mahindi nje ya nchi ili kulima kwa wingi na kuzingatia ubora.