Makamu wa Rais akichambua Kiswahili katika mapenzi


Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema lugha ya Kiswahili ina tuunganisha katika mambo mengi na ina nguvu na nafasi muhimu katika maendeleo ya jamii, siasa na mapenzi.

Samia alisema hayo katika hafla ya utoaji wa tuzo ya Kiswahili ya Mabati- Cornell ya Fasihi ya Kiafrika kwa washindi wa mwaka 2018 iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.

"Kiswahili kinatuunga kwenye mambo mengi, misemo yake inatufundisha uvumilivu na kujenga familia, ukikizungumza vizuri kwa ulimi ulio laini kama wangu. Nikizungumza maneno ya mapenzi kwa Kiswahili unakuja tu, kwa hiyo kinatujenga kuwa ndugu,"alisema.

Tuzo ya fasihi ya Mabati-Cornell ilianzishwa mwaka 2014 ikiwa na malengo ya kuthamini uandishikwa lugha za Kiafrika, kuhimiza sanaa ya tafsiri baina ya lugha za Kiafrika na kutafsiri maandishi ya lugha nyingine kwa lugha za Kiafrika.