Manispaa ya Ilemela yajivunia kuongoza matokeo ya kidato cha nne Mkoa


Na. James Timber, Mwanza

Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeshika nafasi ya kwanza kimkoa na ya 17 kitaifa katika matokeo ya kidato cha nne  mtihani wa Taifa wa mwaka 2008 ambapo jumla ya wanafunzi waliosajiliwa ni 5,106 wasichana wakiwa 2508 na wavulana 2598 na kuchangia ufaulu huo kufikia asilimia 85.4 katika halmashauri hiyo.

Akizungumza katika Kikao cha Baraza la Madiwani mapema hii leo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,  John Wanga alisema kuwa ni jambo la kupongezwa kwa wazazi, walimu, wanafunzi pamoja na Idara ya elimu inayofanya kazi ya kwa ushirikiano na jambo linalochangia  kuimarisha taaluma katika nchi yetu.

Wanga alisema kuwa halmashauri inazo jumla ya shule 47 za sekondari kati yake sule  24 ni za serikali huku  binafsi zikiwa 23, ambapo jumla ya wanafunzi 27,811 tayari wamesajiliwa katika shule za sekondari na serikali kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu.

"Kwa mwaka 2019 wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza ni 8530 kati yao wasichana ni 4421 na wavulana ni 4109, hadi kuishia Februari 8, 2019 wanafunzi 6764 sawa na asilimia 81 ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wameripoti na wanaendelea na masomo katika shule za serikali, huku wanafunzi 1591 ambao ni sawa na asilimia 19 hawajaripoti katika shule walizopangiwa kati yao asilimia 12 sawa na wanafunzi 1024 wameenda shule binafsi na asilimia saba sawa na wanafunzi 567 bado hawajaripoti shuleni, "alisema Wanga.

Aidha aliongeza kuwa shule za sekondari katika halmashauri bado zinakabiliwa na upungufu wa miundombinu na samani ambapo hadi Februari 8, mwaka huu kulikuwa na upungufu wa meza 11,599, viti 16,743 matundu ya vyoo 779, maabara 6 na vyumba vya madarasa 344.

 Alieleza kuwa kutokana na upungufu huo halmashauri imechukua hatua za maksudi hasa kukabiliana na changamoto ya uhaba wa  vyumba vya madarasa kwa kuweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wananchi kuanza ujenzi wa misingi ya vyumba vya madarasa ambapo matofali yanatolewa na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dk.Angeline Mabula ambaye pia ni Naibu wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kisha halmashauri inakamilisha.