Mbunge Sugu awasili Polisi


Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi almaarufu kama 'Sugu' amewasili Ofisini kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya baada ya kupokea wito wa mahojiano.

Sugu ametii wito huo leo asubuhi Februari 21 baada ya Kamanda Ulrich Matei jana kumtaka aemde ofisini kwake.

“Ni kweli tumemuita kwa ajili ya kumhoji kutokana na maneno yake aliyoyazungumza kuhusu Vitambulisho, maana tunaona kunakukashifu na vile ni Vitambulisho vilivyotolewa na Serikali sasa tunapoona mtu anaanza kutoa maneno hayo huo ni uchochezi,” amesema Matei

Kwa upande wake Sugu amesema jana mchana alipigiwa simu na RPC Matei kwamba anatakiwa kufika Ofisini kwake kwa mahojiano kwa kilichoelezwa anataka kuvuruga mchakato wa ugawaji wa Vitambulisho vya Wajasiriamali vilivyotolewa na Rais John Magufuli.

"Nimeitwa kwa amri ya Mkuu wa mkoa kuhusiana na 'clip' yangu nikiwa Iyunga na wajasiriamali waliyokuwa wakielezea changamoto ya Vitambulisho,  Sasa yeye (mkuu wa mkoa) jana sijui alikuwa wapi akatangaza kuna wanasiasa wanataka kuhujumu suala la vitambulisho hivyo, ndio akaagiza Polisi kuwahoji. Sasa kama kutakuwa na jingine sijui maana wamesema wanataka kunihoji," amesema Sugu.

Jana RC Chalamila akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Rungwe alisema kuna wanasiasa wanataka kukwamisha suala la utoaji vitambulisho hivyo na kuwataka kuacha kufanya hivyo kabla hajawachukulia hatua za kisheria.