.

2/14/2019

Mbunge wa Jimbo la Ilemela atimiza ahadi ya Kivuko Bezi


Na James Timber, Mwanza

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula ametimiza ahadi yake aliyoitoa wakati akiomba ridhaa ya kuwa mwakilishi wa wananchi wa jimbo la Ilemela wanaoishi kata ya Kayenze ya kuwahakikishia usafiri wa uhakika kutoka Kayenze kuelekea kisiwa cha Bezi ya upatikanaji wa Kivuko.

Ahadi hiyo imetimia mara baada ya Serikali ya awamu ya tano chini Rais Mhe Dkt John Magufuli kupitia Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi kusikia ombi la mbunge wa jimbo hilo kwa kutenga fedha, kutangaza zabuni na kuanza kwa ujenzi wa Kivuko hicho kupitia kwa mkandarasi Songoro Marine Transport Limited ya Jijini Mwanza inayosimamiwa na wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA iliyoanza ujenzi wa Kivuko hicho utakaokamilika kabla ya mwezi wa Kumi mwaka huu chenye uwezo wa kubeba abiria 250, Tani 85 za mizigo, magari 8 na kuzingatia usasa kulingana na mahitaji ya wakati ambapo Dkt Angeline Mabula amemshukuru Rais Mhe Dkt John Magufuli kwa hatua hiyo huku akiwaomba viongozi na wananchi kuendelea kushirikiana katika kumaliza changamoto zinazowakabili

"Nimefrahi kuona ile ahadi niliyoahidi sasa inaenda kutimia maana tumekuwa tukivutana sana katikati lakini namshukuru  waziri wa eneo husika na mheshimiwa Rais maana ahadi zote tulizozitoa utekelezaji wake ni pale mafungu ya Serikali yanapoimarika," alisema.

Kwa upande wake kiongozi wa kampuni hiyo ya kizalendo na kongwe inayojenga Kivuko hicho Ndugu Major Songoro ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kupata zabuni ya ujenzi wa kivuko hicho na kuahidi kukijenga kivuko hicho kwa ubora, ufanisi, usasa na kukikamilisha kwa wakati ili kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Nae Diwani wa kata ya Kayenze Mhe James Katoro kinakopelekwa kivuko hicho amemshukuru mbunge wa jimbo hilo kwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa kwa wananchi huku akimuahidi ushirikiano katika kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kumaliza kero na changamoto za wananchi.