Mkurugenzi mikononi mwa Polisi kwa tuhuma za mauaji


Jeshi la Polisi Mkoani Singida linawashikilia watu watano akiwamo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Pius Luhende kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mfugaji Peter Chambalo, anayedaiwa kupigwa risasi akiwa kanisani.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Ahmed Msangi alikiri kutokea kwa tukio hilo juzi na kueleza kuwa mpaka sasa, wanaoshikiliwa ni watu wa watano akiwamo mkurugenzi huyo.

Msangi alitaja watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa kuwa ni askari wa wanyamapori wawili, mmoja kutoka Mamlaka ya Wanyamapori (Tawa) na mwingine kutoka Halmashauri ya Ipigi, mwanasheria na mtendaji wa kata.

“Ni kweli tukio limetokea, lakini siyo kweli kuwa askari wa Jeshi la Polisi wamehusika na tukio hilo," Msangi alisema, "kwanza hawakuwapo kwenye tukio hili.

"Waliokuwapo ni askari wanyamapori, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, mwanasheria wake na mtendaji wa kata. Kilichotokea ni kwamba, walipofika katika kijiji cha Kazikazi, Kata ya Kitaraka, Tarafa ya Itigi, kulitokea kutoelewana, hivyo kusababisha vurugu," alisema.

Aliongeza kuwa, wakati wa vurugu hizo, inadaiwa askari walifyatua risasi na kumjeruhi mtu huyo ambaye alifariki dunia.