https://monetag.com/?ref_id=TTIb Njia za kutatua mtafaruku katika mahusiano ya kimapenzi | Muungwana BLOG

Njia za kutatua mtafaruku katika mahusiano ya kimapenzi

Migongano na tofauti kati ya watu wawili katika mahusiano ni kitu kisichoepukika iwe ni mahusiano ya mapenzi ,mahusiano ya mzazi na mtoto na hata mahala pa kazi. Sababu za mifarakano katika mahusiano ziko wazi; kwamba watu hawa wametoka na kukulia katikia mazingira tofauti na hivyo tabia na hulka zao ni lazima zitatofautiana.

Katika hali kama hii migongano na kutoelewana wakati mwingine ni vitu ambavyo vinatokea na kunahitajika busara na mbinu mahususi za kukabiliana na tatizo hili

1. Kuwa wa kwanza kuchukua hatua
Kunapotokea kufarakana kati ya watu wawili kwa kawaida mawasiliano huvunjika au kuwa magumu na mabaya. Kila mmoja anaweza akwa na kinyongo na mwingine. Kwa wapenzi hali hii inaweza ikawa ya kuumiza zaidi kwani inahusisha hisia kwa kiasi kikubwa;ni jukumu lako wewe kufunja ukimya na kuwa wakwanza kuleta suluhu.

Tafuta nafasi na omba kujadili na kuongea kuhusu tofauti zenu.

2. Anza kwa kuangalia kosa lako kwanza
Ni kawaida katika ugomvi na mifarakano kwa mmoja kumuona mwenzake kuwa ndiye mkosaji,na kusahau kuwa huenda kosa likawa upande wake pia. Kama suala hilo limemuudhi mwingine pia huenda kuna tatizo toka kwako pia,au labda yeye anaona kuna tatizo upande wako.

Kutambua hilo unahitaji kujihakiki mwenyewe kwanza na kumsikiliza mwenzio kama ana hisia gani. Kama utaona kuna shida upande wako pia basi ni wakati wa kuomba msamaha kwa nafasi yako kwanza.

3. Sikiliza kwa umakini shida na mtazamo toka upande wa pili-vaa viatu vyake
Inasemwa kuwa sababu kubwa ya malumbano na ugomvi ni kuwa tunataka kusema zaidi kuliko kusikiliza upande wa pili,na kwa kufanya hivyo tunakuwa wabinafsi.

Ukisikiliza vizuri toka upande wa mwingine na kujaribu kusikia hisia zake huenda ukaliangalia jambo husika katika namna nyingine ambayo itapelekea maelewano. Ni muhimu sana kuonesha kuwa unajali hisia zake.

4. Kuwa mkweli na maanisha unachokisema-sema toka moyoni
Mdomo unaweza kutamka chochote bila kumaanisha,kweli hutoka moyoni. Unaposema kitu kwa hisia na kwa dhati unasikika zaidi. Ongea toka moyoni na maanisha unachosema na matokeo yake yatakuwa mazuri.

5. Jizatiti katika kusuluhisha tatizo na sio kulaumu
Lawama hazisaidii kuleta suluhisho la tatizo mbele yenu,ukweli ni kuwa linasababisha upande wa pili kujihami,ni asili kwa mtu anayeshambuliwa kujihami hali kadharika katika mazungumzo.

Badala ya kulaumu ni vyema kama mtaangalia tatizo lenyewe ni nini na mzizi wake.

6. Kazania katika kupata maelewano na sio kumaliza tofauti zote
Si kitu rahisi mkamaliza tofauti zenu kwa kuwa ni watu wawili mliotoka katika mazingira yasiyofanana,badala yake mukubaliane namna ambazo mtaishi kwa amani na kuheshimu hisia na nafasi ya mwingine.

Kuwa tayari kukubaliana kutokubaliana katika baadhi ya mambo. Maelewano ndio jambo la msingi katika kuleta suluhu.

7. Kazania katika kuonesha kipi ni sahihi na sio nani yuko sahihi
Katika mifarakano si vyema kumtaja mwingine kuwa hayuko sahihi,kwasababu ya kwanza ni kuwa huenda wewe mwenyewe ukawa hauko sahihi lakini ya pili ni kuwa huko ni kurusha makombora ya lawama ambako kutamfanya mwingine kujihami na hivyo kutofikia maelewano.

 Jambo la mwisho la kuzingatia
Mnapotafuta suluhisho la ugomvi au mfarakano katika mahusiano ni muhimu kuzingatia vitu viwili vikubwa,kuondoa ubinafsi na kujishusha. Kwasababu ukosefu wa vitu hivi viwili ndio sababu kubwa katika mifarakano yote.

Na msingi upo katika kusikiliza hisia za mwingine. Usikivu ni bora zaidi kuliko kusema,unaposikiliza unaonesha kujali zaidi na inakuwa rahisi kufikia maelewano na kumaliza ugomvi na mifarakano katika mahusiano yoyote.