RC Ayoub atoa siku moja kwa wauzaji wa Mchanga na Mawe


Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi, imewapa siku moja wafanyabiashara wa magari ya uuzaji mchanga na mawe katika eneo la Mwanakwerekwe,Welezo,Chuwini na Kisauni kuhama maeneo hayo na kuhamia eneo la Jumbi.

Imesema hatua hiyo ni agizo kutoka serikali na kwamba kwa watakaokiuka agizo hilo vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa vitachukua hatua kali.

Akizungumza jana na wanachama wa jumuiya ya mchanga na mawe, Mwanakwerekwe Mkuu wa Mkoa huo Ayoub Mohammed Mahmoud alisema serikali imetoa agizo hilo kutokana na kuwa mji huo unaendelea kukua na kwamba shughuli za biashara hizo zinapaswa kufanyiwa nje kidogo ya mji.

Mkuu huyo aliongeza kuwa kutokana na mji kuwa mdogo huku maendeleo ya mji huo ikiwa inaongezeka mara dufu ndipo serikali ikaona ifanya hatua hiyo ya kuwahamisha na kuwatafutia eneo hilo.

"Kuanzia kesho vyombo vya ulinzi na usalama vitafanya kazi ya ukaguzi wa maeneo hayo ambayo nimeyataka wafanyabiashara hao wahamie na watakao kiuka vyombo vya ulinzi na usalamavitatumia nguvu na kwamba ieleweke kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la serikali,"alisema Mkuu huyo wa Mkoa

Katika maelezo yake Mkuu huyo wa Mkoa alisema maeneo ni hayo ni madogo na wafanyashughuli hizi wapo zaidi ya watu 500 hadi 600 na kusababisha kuwepo kwa magari mabovu katikamaeneo hayo na kuwepo na gereji bubu.

Alisema agizo la serikali lazima litekelezwe hivyo watu wote walioko katika maeneo ya Chuwini,Welezo,Kisauni na Mwanakwerekwe lazima wahamie jumbi na kwamba huku katika ya mji hakutakuwa na shughuli hizo tena.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mchanga na Mawe, Idd Hame, alisema kutokana na agizo hilo kutoka serikalini lakini bado serikali ya mkoa imefanya busara kutafuta eneo lingine hivyo hakuna budi kutekeleza agizo hilo.

Alisema baada ya kuhamia huko katika eneo la Jumbi utaratibu wa kuwa wanajumuiya ambao wamesajiliwa tu na jumuiya hiyo ndio watakaoruhusiwa kufanya shughuli zao katika eneo hilo.

"Tunajua kuna baadhi ya watu bado hawajajisajili hivyo tunatoa siku tatu tu kwa wote ambao hawajajisajili wawe tayari na hivyo tukihamia huko tunatakiwa tuwe na vitambulisho na hasiyekuwa navyo hatorusiwa kufanya shughuli hapo,"alisema.