Serikali haitamlipa Kangomba - Waziri Hasunga


Sheria ya Korosho kifungu cha 12 hakimruhusu mtu yeyote kufanya kazi ya korosho pasina kutambulika, wakati kifungu cha 15 cha sheria hiyo katika kifungu kidogo cha nne kinawataka wahusika wote wa korosho wawe wamesajiliwa na kuwa na leseni ya biashara hiyo.

Bila kuwa na usajili huo kwa mfanyabiashara yeyote wa korosho ni kosa kisheria hivyo kwa atanayebainika anapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Serikali imetilia msisitizo maagizo iliyoyatoa hivi karibuni kuwa katika malipo ya wakulima wa korosho haitamlipa mfanyabiashara asiyetambulika kisheria (Kangomba).

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameyasema hayo wakati akizungumza na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Pwani.

Hasunga amesema kuwa ni lazima sheria zifuatwe katika utekelezaji wa majukumu yote ikiwemo biashara ya zao la korosho ili kuwanusuru wakulima wanaotumia nguvu nyingi katika kilimo hicho huku wakipata matokeo duni kutokana na baadhi ya wafanyabiashara wanaowahujumu (Kangomba).

Ameongeza kuwa wahujumu katika biashara za mazao mbalimbali ya kilimo nchini katika kipindi kirefu wamekuwa wakiwanyanyasa wakulima kwa kuwanyonya katika bei jambo ambalo serikali imelibaini hivyo kuingilia kati.

Aliongeza kuwa sababu ya wakulima kuchelewa kulipwa fedha za korosho zao kutokana na uhakiki uliochukua muda mrefu umesababishwa na vyama vya Ushirika kutofanya kazi yao ipasavyo kwa kuwasajili na kuwatambua wakulima.

“Vyama vya ushirika ndivyo vinapaswa kuwajua na kuwatambua wakulima wake katika mazao yote yanayouzwa kupitia mfumo huo, vinginevyo kutofanya kazi kwa weledi kumetuchelewesha kwa kiasi kikubwa” Alikaririwa Hasunga na kuongeza kuwa“Hata sheria yetu ya maghala haikufanya kazi vizuri, Vyama vya msingi havikutekeleza majukumu yake".

Hasunga amesema kuwa serikali haitawavumilia wote wanaofanya biashara hiyo kinyume na sheria badala yake watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameanza ziara ya kikazi mkoani Pwani, Lindi na Mtwara ambapo katika ziara hiyo atafuatilia mwenendo wa malipo ya wakuli wa zao la korosho.