https://monetag.com/?ref_id=TTIb SMZ yakabidhiwa hati ya kiwanja cha heka 30 Mji wa serikali | Muungwana BLOG

SMZ yakabidhiwa hati ya kiwanja cha heka 30 Mji wa serikali


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameikabidhi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) hati ya kiwanja chenye ukubwa wa heka 30 kilichopo Mji wa Serikali Jijini Dodoma kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi Jijini humo.

Makabidhiano hayo yamefanyika wakati wa kikao cha kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kujadili masuala ya Muungano kilichofanyika Jijini Dodoma.

"Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tunawakaribisha Dodoma, wenzenu tumeanza na nyie tunawategemea kuwepo Dodoma,” amesema Makamu wa Rais.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema kiwanja kilichokabidhiwa kwa SMZ kina ukubwa wa sawa na viwanja kumi vilivyogawiwa kwa Wizara, kwani viwanja vya Wizara vinaukubwa wa kati ya heka 3 hadi 5 kwa kila wizara.

Ameendelea kusema, utoaji hati kwa SMZ ni muendelezo wa utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhamishia shughuli zake Jijini Dodoma, ambapo tayari wizara zote zimekwisha hamia Jijini humo na mwezi huu zinatarajia kuhamia Mji wa Serikali, uliojengwa eneo la Ihumwa.

Aidha Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameshatoa hati za viwanja kwa Balozi zote zilizopo hapa nchini ili nazo zihamie Jijini humo ambayo ndiyo Makao Makuu ya Nchi.