SMZ yawataka wafanyabiashara kuokoa Mazingira


Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein amefanya ziara katika miradi mbalimbali na kutoa maagizo juu ya utekelezaji kwa baadhi ya wizara, ikiwa ni pamoja na kuangazia maeneo kadhaa ikiwemo suala la mazingira.

Akikagua maeneo yanayotegemewa zaidi kwa upatikanaji wa rasilimali ya madini ya mchanga katika machimbo ya Pangatupu pamoja na Chechele, Dkt. Shein amesema “Mchanga katika mashimo haya umepungua kwa asilimia kubwa jambo ambalo linakwamisha baadhi ya miradi pamoja shughuli za ujenzi wa nyumba za wananchi kukwama”.

Aidha, Dkt. Shein, amewaeleza wananchi namna rasilimali ya mchanga ilivyopungua na kutaka wanachi kushirikiana na Serikali kupanga mikakati kabambe ambayo itawezesha kutunza rasilimali hiyo ili iweze kutumika kwa uangalifu mpaka pale suluhisho sahihi litakapo patikana.

Dkt. Shein amezitaja sababu ya kupungua kwa rasilimali hiyo kuwa ni pamoja na kutofuatwa kwa sheria za nchi na sasa kuchangia uhaba wa rasilimali hiyo kuwepo visiwani hapo. Pia,wengine wanadaiwa kutumia kama njia ya kujichukulia mchanga bila utaratibu maalum.

Akifafanua kuhusu maeneo hayo, Dkt Shein ameongeza kwa kusema kuwa, mashimo ya Pangatupu yanakadiriwa kuwa ekari 64, na jumla ya tani 50,000 zilizobakia na mchanga,ambapo   mashimo ya Chechele yana jumla ya tani 2,000 ambazo zinategemewa kwa ajili ya miradi ya Serikali kama ujenzi wa hospitali, shule, masoko pamoja na ofisi.

Aidha,Dkt Shein amesema athari zimeanza kuonekana mfano miradi mkubwa kama ujenzi wa jengo la Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) umekwama kutokana na ukosefu wa mchanga na jambo hili limepelekea mkakandarasi kusitisha ujenzi mpaka pale atakapopata rasilimali ya mchanga. Mradi wa ZURA unategemewa zaidi kutoa huduma kwa wakazi wa Zanzibar, ambapo inasimamia miradi mikubwa muhimu.

Vilevile kuna athari za kimazingira kwa kuwa mashimo hayo kipindi cha mvua yanajaa maji ambayo sio tu yanahatarisha maisha ya watu hususan watoto na wanyama lakini vilevile, yanakuwa mazalia ya mbu na kujenga mazingira ya kuibuka maradhi yakiwemo ya milipuko kama homa ya matumbo ya kuharisha na wakati mwingine kupelekea kipundupindu.

Ipo haja ya wafanyabiashara kote nchini kuwasiliana na wahusika na kutazama jambo hili kwa mtazamo wa kuokoa mazingira na kuhakikisha shughuli za maendeleo zinatekelezwa bila kukwama. Wafanyabiashara hao wana uwezo wa kuhakikisha wanatafuta rasilimali ya madini ya mchanga  ili kuweza kunusuru rasilimali ya mchanga iliyopungua Zanzibar.