TAKUKURU na Uhamiaji wawaomba wanafunzi jambo hili


Na. Ahmad Mmow, Nachingwea.

Katika kuhakikisha mapambano dhidi ya rushwa yanafanikiwa na elimu ya uraia inafikishwa kwa jamii, Wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari zilizopo Wilayani Nachingwea wameombwa kufikisha kwa jamii elimu wanayopata kuhusu uraia na vita dhidi ya rushwa.

Wito huo umetolewa leo mjini Nachingwea  na Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) na Idara ya Uhamiaji, kwanyakati tofauti katika shule za msingi za Juhudi,Nachingwea, Mianzini, Majengo na Ilulu.

Ofisa wa TAKUKURU,Ines Kizindo alisema elimu inayotolewa shuleni kuhusu madhara ya rushwa na faida ya kukomesha tatizo hilo kubwa katika utoaji na upatikanaji wa haki,hainabudi kufikishwa kwa jamii kupitia kwa wanafunzi na wadau wengine.Huku taasisi hiyo ikiendelea kutoa elimu hiyo shuleni na katika makundi mengine ya kijamii.

Aliwaomba wanafunzi kusaidia kuwakumbusha wazazi na walezi wao kuhusu madhara ya rushwa na kutoa taarifa kwa taasisi hiyo pindi wanapoona kunadalili za kufanyika vitendo vya rushwa dhidi yao na jamii kwa jumla.

"Wanafunzi muwe tayari kufikisha elimu mnayopewa,pia kuwe na ari ya kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa,"alisema Kizindo.

Kwa upande wake, Ofisa wa Idara ya Uhamiaji, Augustino Chonya alisema japokuwa elimu ya urai inafundishwa shuleni,hata hivyo kuna changamoto ya wananchi kutojua mambo yanayohusu uraia. Hivyo kuna umuhimu mkubwa wa elimu hiyo kufikishwa kwa jamii.

Chonya alisema raia ndio wenye nchi,kwahiyo wanahaki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa viongozi katika nchi yao.Hivyo mtu ambae sio raia anapochaguliwa kuwa kiongozi ni rahisi mtu huyo kusimamia na kutetea masilahi ya nchi anayotoka.

Alisema raia wasipotambua haki na wajibu wao wanaweza kuwakaribisha wageni wasio na nia njema.Hali inayoweza kusababisha madhara makubwa kwa nchi.Ikiwamo usalama wa nchi kuzorota.

"Raia wasipotambua haki zao wanaweza kujiingiza na kujihusisha na vitendo vya kihalifu kutokana na kuiga tamaduni na mila za nchi nyingine bila kujua madhara yake," alisema Chonya.

Lengo ya ziara hiyo ni kuhamasisha uanzishaji wa vilabu vya kuzuia na kupambana na rushwa katika shule za msingi.Nibaada ya kufanya hivyo na kufanikiwa kuanzishwa vilabu kama hivyo katika shule za sekondari.