.

2/12/2019

Tanzania yatajwa kufanya vizuri mapambano dhidi ya rushwa


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema nchi za Bara la Afrika zimeitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa. Mbali na hilo, pia amesema ripoti ya kamati maalumu iliyoundwa kuhusu masuala ya afya inaonesha Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri.

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akitoa muhtasari wa yaliyojiri kwenye Mkutano wa 32 wa Wakuu wa nchi za Afrika (AU) unaofanyika Addis Ababa, Ethiopa.

Amesema katika mkutano huo pamoja na mambo mengine Serikali barani Afrika zimesisitizwa kupambana na wala rushwa, ambapo Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika mapambano hayo.

“Imetupa faraja kwa sababu ukaguzi uliofanywa na kamati maalumu ya maendeleo ya afya, iliyotembelea nchi za Afrika kuona mwenendo wa utoaji wa huduma za afya imeonesha kwamba Tanzania tupo kwenye kiwango kizuri,” amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesema Tanzania imefanya vizuri katika kusimamia na kudhibiti malaria, mapambano dhidi ya ukimwi pamoja na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi mpaka vijijini. Mafanikio hayo yamekuja baada ya Serikali kuongeza bajeti ya afya wizara kutoka sh. bilioni 37 hadi kufikia sh. bilioni 269.