Ulipofikia mradi wa reli ya kisasa (SGR), serikali yatia neno


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa treni ya kwanza kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro inatarajia kuanza safari zake Novemba mwaka huu kama kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.

Amebainisha hayo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Reli kwa kiwango cha kimataifa (SGR)kutoka Dar es Salaam hadi eneo la Soga, umbali wa kilometa 53.

"Ninampongeza sana Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake kubwa na kuamua kwa dhati kutekeleza mradi huu mkubwa na miradi mingine, ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji ya Mto Rufiji, ambayo kukamilika kwake kutachochea uchumi wa viwanda" alisema Naibu Waziri huyo.

Kwa sasa ujenzi wa reli hiyo imefika Dar es Salaam eneo la Vingunguti ambapo Naibu Waziri ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi na kumpongeza mkandarasi, kampuni ya Yapi Merkezi.