Wakati wa mkutano wa AU Guterres asifu mafanikio ya Afrika


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameuhutubia mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika ambapo amesifu mafanikio katika chaguzi za hivi karibuni, mikataba ya amani na jinsi Afrika inavyowashughulikia wakimbizi.

Wakati wa hotuba yake iliyojaa matumaini Guterres aliunga mkono juhudi za bara la Afrika katika kuifungua mipaka na milango yake na kuonesha mshikamano wa hali ya juu katika kuwasaidia wakimbizi.

Gutteres aliwaambia viongozi wa Afrika na wanadiplomisia wa ngazi ya juu wanaohudhuria mkutano huo kuwa katika juhudi za kutafuta suluhisho la kudumu kwa tatizo la wakimbizi bara la Afrika limekuwa kielelezo cha maana kwa ulimwengu na kwa chombo anachokiongoza.

Kuhusu Afrika inavyojitoa katika kusaidia suala la wakimbizi Guterres amesema "Licha ya changamoto binafsi za kijamii, kiuchumi na kiusalama, serikali za afrika na watu wake zimefungua mipaka, milango na mioyo yao kwa mamilioni ya watu wenye uhitaji.”

Afrika ndiyo inahifadhi zaidi ya theluthi ya wakimbizi na watu walioyahama maskani yao kote ulimwenguni.

Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesifu pia juhudi za kusaka amani katika mataifa ya Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati pamoja ya kuyapongeza mataifa ya Mali, Madagascar na DR Congo ambayo yalifanya uchaguzi hivi karibuni.