Asilimia 80 ya Wananchi kutumia Bima ya afya Simiyu


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amesema mkoa huo umejiwekea malengo ya kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wake kuwa na kadi za bima ya afya ili kujihakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu katika vituo vya kutolea huduma za afya hapa nchini.

Mtaka ameyasema hayo wakati ufunguzi wa Jukwaa la Ushirika Afya Mkoa wa Simiyu lililofanyika kwa lengo la kujadili namna wanachama wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS)wanavyoweza kujiunga na Bima ya afya na kupewa kadi kupitia vyama vyao na kama familia, ambalo limefanyika Machi 14, mjini Bariadi.

Amesema yeye kama Mkuu wa Mkoa atafanya vikao na wanachama wa AMCOS na makundi mbalimbali ya wananchi katika wilaya zote mkoani hapa na kuzungumza nao kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kila mwananchi kuwa na Bima ya Afya kwa ajili ya matibabu.

Aidha, amesema atawaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuwa katika Vyama vya Ushirika Vya Msingi ambavyo vinawapa nafasi ya kupata Bima ya afya na kupata matibabu makubwa katika vituo vya kutolea huduma za afya vya binafsi na vya umma kwa gharama nafuu ya shilingi 76,800/= kwa mtu mmoja(mwanachama wa ushirika).

“Nitafanya vikao na wanachama wa AMCOS zote, wakulima, wafugaji, wajasiriamali, makundi yote ya wananchi kwenye mkoa wetu wa Simiyu, tuweze kuwaelimisha faida ya mwananchi wa mkoa wa Simiyu kuwa na bima ya afya, kubwa zaidi umuhimu wa kuwa kwenye ushirika ambao utamwezesha kupata matibabu makubwa kwa bei nafuu” alisema.

Katika hatua nyingine Mtaka amesema katika kipindi cha msimu wa pamba kila kituo cha kununulia pamba NHIF itaweka Afisa wake kwa ajili ya kusajili wakulima na wanachama wa vyama vya ushirika walio tayari, hivyo akatoa wito kwa viongozi walioshiriki jukwaa la ushirika afya kutoa taarifa na elimu kwa wenzao juu ya umuhimu wa suala hilo.

Mtaka pia ametoa wito kwa wakulima wote wa pamba kulipa kipaumbele suala la afya kwa kuchukua hatua ya kuwa na bima za afya ili waweze kuona manufaa ya Serikali kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Hospitali za wilaya kwa kila wilaya na Vituo vingine vya kutolea huduma za afya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernad Konga amesema NHIF ni wadau wakubwa mkoani Simiyu, hivyo wako tayari kutoa huduma bora na watawafikia wananchi wa makundi yote mkoani hapa na watahakikisha wanatoa kadi za bima ya afya kwa wakati kwa wanachama wote watakaojiunga.