Korea Kaskazini yataka vikwazo dhidi yake vilegezwe


Korea ya Kaskazini imesema leo kuwa hakuna uhalali wa kuendeleza vikwazo kamili dhidi yake, ikizingatiwa kuwa imeshasitisha majaribio yake ya makombora na zana za nyuklia miezi 15 iliyopita.

Ju Yong Chol ambaye ni mwanadiplomasia wa Korea Kaskazini amesema suala hilo kati ya nchi yake na Marekani linapaswa kutatuliwa baina yao ili kujenga uaminifu.

Yong Chol alisema hayo alipojibu hotuba iliyotolewa na afisa mkuu wa kudhibiti silaha wa Marekani wakati wa mkutano uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa kuhusu uondoshaji wa silaha.

Katika mkutano wa kilele kati ya Marekani na Korea Kaskazini uliofanyika mwezi uliopita mjini Hanoi, kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na rais wa Marekani Donald Trump hawakuelewana kufuatia hoja iliyoibuka kuwa vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini haviwezi kulegezwa kabla ya kuondolewa kwa silaha za nyuklia.