Machi 31 Wakulima wote wa Korosho watakuwa wamelipwa fedha zao


Wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wamehakikishiwa kuwa kufikia tarehe 31 Machi mwaka huu Wakulima wote watakuwa wamelipwa fedha zao kwani uhakiki umekamilika kwa kiasi kikubwa.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametoa hakikisho hilo mbele ya kamati hiyo katika ukumbi wa mikutano kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi wakati akitoa ufafanuzi katika mkutano uliowakutanisha wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wake Dkt Christine Ishengoma, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Naibu Katibu Mkuu wizara ya Kilimo, wataalamu serikalini sambamba na wakulima.

“Kumekuwa na urasimu mkubwa tangu kuanza kwa zoezi hili la uhakiki lakini sasa tumeamua kama serikali kabla ya mwisho wa mwezi huu wa tatu wakulima wote wawe wamelipwa malipo yao ili kuondoa adha wanazokumbana nazo” alikaririwa Mhe Hasunga

Alisema pamoja na kwamba malipo ni mchakato unaohitaji kupitia katika hatua nyingi za mchakato ikiwemo uhakiki lakini kila jambo lenye mwanzo ni lazima kuwa na ukomo.

Alisema mpaka sasa Tani 222,684 zimekwisha kusanywa huku hadi kufikia tarehe 14 Machi 2019 tayari jumla ya Shilingi Bilioni 596.9 zimekwishalipwa kwa wakulima kati ya Shilingi Bilioni 723

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga amewahakikishia wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuwa pamoja na mchakato huo wa malipo ya Korosho kuendelea lakini pia Wizara imepitia katika michakato mbalimbali ya kumpata Mkurugenzi mpya wa Bodi ya Korosho ili kuendelea na majukumu ya Bodi hiyo.

Kuhusu wanaofanya biashara ya zao hilo kinyume na sheria maarufu kama Kangomba Waziri Hasunga alisema kuwa tayari serikali imewabaini na wote watachukuliwa hatua za kisheria.