Maeneo ya msumbiji yakosa umeme na maji kufuatia kimbunga Idai


Baadhi ya raia wa Msumbiji bado hawana umeme na maji siku chache baada ya kimbunga Idai kupiga baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na nchi jirani za kusini mwa Afrika.

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amesema huenda idadi ya waliokufa kutokana na kimbunga hicho ikafika 1,000.

 Idadi rasmi ya waliokufa nchini humo kwa sasa ni watu 84. Kimbunga Idai kiliuathiri zaidi mji wa Beira, huku shirika la Msalaba Mwekundu na Hilal Nyekundu yakiripoti kwamba uchunguzi wa angani unaonyesha kuwa asilimia 90 ya majengo yameharibiwa.

 Shirika la Msalaba Mwekundu pia limekadiria kuwa kimbunga hicho kilichosababisha mafuriko kimewaacha watu 400,000 bila makao.

Nchi nyingine zilizoathiriwa na kimbunga hicho ni Malawi na Zimbabwe ambapo zaidi ya watu 100 wameuawa na zaidi ya 200 hawajulikani walipo.