Makusanyo ya kodi kwenye dhahabu yaongezeka Geita, yafikia Tsh. Bilioni 114.78


Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Pro. Simon Msanjila amesema kati ya mwaka 2011 hadi 2018, kiwango cha ukusanyaji wa maduhuli katika sekta ya madini mkoani Geita kimeongezeka kutoka Tsh. Bilioni 24 hadi 114.7.

Amesema mafanikio hayo yamechagizwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ikiwamo mabadiliko ya kisheria kwa lengo la kuongeza manufaa ya rasilimali hiyo kwa Taifa.

Pro. Msanjila ametoa kauli hiyo leo Jumapili Machi 17, 2019 wakati akihutubia katika tukio la uzinduzi wa soko la kwanza la madini hapa nchini.

Pamoja na mafanikio hayo katika ukusanyaji maduhuli, Profesa Msanjila amesema shughuli ya maandalizi ya upatikanaji wa maeneo ya masoko inaendelea kwenye mikoa mbalimbali.

“Tayari kazi ya kutenga maeneo inaendelea, wanaangalia vigezo vya kiusalama lengo ni kuhakikisha kila mkoa wenye madini unapata soko la madini,” amesema Pro. Msanjila.

Uzinduzi wa soko hilo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilotoa Januari 22, jijini Dar es Salaam mwaka huu kupitia mkutano wake na wafanyabiashara wa madini