Mambo muhimu unayopaswa kuyatawala katika safari yako ya mafanikio

Ushindi wowote katika mafanikio unapatikana kwa kutawala. Kwa mfano, Ili uweze kufanikiwa katika biashara unatakiwa kuitawala biashara hiyo katika kila eneo, kwa kuijua biashara hiyo ndani nje tena kwa uhakika.

Hata katika mafanikio kwa ujumla vipo vitu ambavyo unatakiwa kuvitawala, kwa jinsi unavyovitawala vitu hivyo unapata uhakika wa mafanikio kwa asilimia kubwa sana. Je, ni mambo yapi ambayo unatakiwa kuyatawala ili kufanikiwa?

1. Jitawale wewe kwanza. 
Kitu cha kwanza ambacho unatakiwa kukitawala vizuri ili ujijengee mafanikio ni kujua jinsi ya kujitawala wewe. Tambua jinsi ya kutawala fikra zako, matendo yako, vitu unavyosoma au kuangalia, imani na mitazamo uliyonayo juu ya maisha ya mafanikio.

Kwa kujua jinsi ya kutawala hayo mambo inakusaidia sana wewe kuweza kufanikiwa na kupiga hatua. Watu wanaofanikiwa wanajua sana jinsi ya kujitawala wao wenyewe hasa kutokana na kumudu kutawala mambo kama hayo kila wakati.

2. Tawala mihemko yako. 
Kujitawala wewe tu hiyo haitoshi, ni muhimu kujua jinsi ya kutawala mihemko yako. Huwezi kufanikiwa kama unashindwaa kutawala mihemko yako. Hapa inabidi ujue kutawala tamaa zako au kujizuia kwa mambo yanayokuangusha kimafanikio.

Kama ukishindwa kutawala mihemko yako ni wazi utashindwa. Ipo mihemko ya aina tofauti kama mihemko ya kununua vitu hovyo, au mihemko anasa zisizo na mbele wala nyuma. Kikubwa jiangalie una mihemko ipi wewe inayokuangusha?

3. Tawala visingizio vyako. 
Kila wakati fanya ufanyalo, lakini hakikisha  usiwe tu mtu wa visingizio, tawala visingizio vyako na kila aina ya visingizio weka pembeni. Usiwe mtu kila unaposhindwa jambo unasingizia kwamba umeshinsddwa kwa sababu hii au ile.

Kama jambo umeshindwa kweli ni bora ukaa kimya na uache kusingizia singizia vitu kwani huwezi kukosa sababu. Ukiweza kutawala sababu zako, ukiweza kutawala visingizo vyako, basi anza kujihakikishia mafanikio yako.

4. Tawala maono yako.
Najau zipo ndoto au maono ambayo unayo na kila  siku unaomba Mungu hayo maono yako yaje yatimie. Sasa jifunze jinsi yakutawala maono yako. Maono hayo yaweke kwenye karatasi au picha na ikiwezekana uwe unayaona mara kwa mara.

Weka utaratibu wa kujikumbusha kila siku na kwa kujikumbusha huko inakusaidia kutawala sana maono hayo kwa sehemu kubwa. Wengi wanaoshindwa kufanikiwa, ni watu ambao kiuhalisia wanashindwa kutawala maono yao kwa sehemu kubwa sana.

5. Tawala sheria za mafanikio. 
Hata kama hujui lakini naomba nikwambie kwamba, zipo sheria zinazotawala mafanikio unayoyatafuta. Kwa bahati mbaya sana sheria hizo zinafanya kazi eidha uwe unajua au hujui lakini sheria hizo zipo kazini muda wote.

Wale wanaoshindwa ni watu ambao wanashindwa sana pia kumudu kutumia sheria za mafanikio. Unatakiwa kujua jinsi ya kutawala sheria za mafanikio ili ziweze kukupa mafanikio ya uhakika. Ukishindwa kufanya hivyo ujue utakwama kufikia ndoto zako.

6. Tawala watu wanaokushauri.
Kila mtu ana mtu anayemshauri katika jambo fulani hivi liwe la mafanikio au la kawaida. Wengi sasa kwa bahati mbaya wana washauri wabovu, yaani wanashauriwa na watu wasio sahihi kwa lugha nyingine watu hao wanawapoteza.

Kwa hiyo ili kufanikiwa kitu ambacho unatakiwa kukitawala vizuri na kukipe mafanikio ni kutawala washauri. Tafauta washauri ambao watakusaidia wewe kufanikiwa na si washauri watakokupoteza wewe na kukufanya uonekane hufai.

7. Tawala muda wako. 
Kutawala muda ni jambo gumu sana kwa watu wengi kulifanya. Watu wengi wanashindwa kutawala muda wao na matokeo yake muda wanaupoteza sana kwa mambo ya hovyo ili mradi tu muda huo umepotezwa pasipo malengo.

Kwa mfano; kuna wanaopoteza muda wao katika soga, kuna wanaopotezea muda wao kufanya kazi ambazo si zao badala wangefanya kazi zao ambazo zingewapeleka na kuwapa mafanikio makubwa ya kimaisha kwa sehemu kubwa sana.

8. Tawala mipango yako. 
Ile mipango uliyonayo hautakiwi kuiacha tu hivi hivi hewani, unatakiwa kujua jinsi ya kuitawala mipango yako na ukapata mafanikio makubwa. Kila wakati jikumbushe mipango yako ni ipi na utaifatilia vipi hadi ifanikiwe.

Unapokuwa unajua hatma kama hizi za mipango uliyonayo, hicho ni kichochezi cha kukupa wewe nguvu ya kuweza kusonga mbele zaidi kwenye mafanikio. Watu wengi wenye mafanikio wana uwezo wa kutawala pia mipango yao sana na kuimudu.

Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatimia