Mimi ni Waziri wa vitendo, ninafanya hivi kwa lengo moja tu.. - Waziri Lugola


Na Felix Mwagara, Morogoro

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amefanya operesheni kubwa ya kukagua na kupima ulevi wa pombe kwa madeveva wa mabasi na malori mjini Morogoro leo.

Ukaguzi wa mabasi na malori hayo ulifanyika barabara kuu itokayo Dodoma kuja Morogoro-Dar es Salaam ambapo Waziri huyo akiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa huo (RPC), Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa huo (RTO), alisimamisha vyombo hivyo vya moto vilivyokuwa vinaingia Mizani iliyopo eneo la Kihonda, nje kidogo ya Mji wa Morogoro.

Akizungumza na madereva, kondakta, wapiga debe na abiria mara baada ya kufanya ukaguzi huo, Lugola alisema ni wajibu wake kufanya hivyo katika hatua ya kupunguza kwa kasi ajali mbalimbali zinatokana kwa uzembe wa madereva nchini.

“Mimi ni Waziri wa vitendo, nikiagiza nataka nitekelezwe, na pia nikiahidi lazima nilifuatilie, niliwaambia nitakua nakuja kufanya ukaguzi muda wowote ambao hamuujui, na ninafanya hivi kwa lengo moja tu, kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa ikiwa ni hatua ya kumaliza kupunguza au kumaliza kabisa ajali za barabarani hapa nchini,” alisema Lugola.

“Madereva wa mabasi na malori ambao nimefanikiwa kuwapima kilevi leo wasiopungua sita sijawakuta na kilevi, wapo makini na hii inaleta nguvu na imani kuwa madereva wanaelewa na kuzingatia sheria za usalama barabarani,” alisema Lugola.

Aliongeza kuwa kwasasa ajali zimepungua nchini hasa Mkoa wa Morogoro, kwa sababu ya askari wa usalama barabarani kufanya kazi zao kiweledi, na pia madereva kufuata sheria za usalama barabarani.