Pep Guardiola kutimkia Juventus.


Mhispania Pep Guardiola, Kocha wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Manchester City (48), amefikia makubaliano na uongozi wa klabu ya Juventus kwa ajili ya kuisimamia timu hiyo kwa mkataba wa miaka minne.

Inadaiwa kwamba, kocha wa Juventus, Massimiliano Allegri, anatarajia kuondoka mara baada ya kumalizika kwa msimu huu ili kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine, hivyo kwa mujibu wa mwandishi kutoka nchini Italia, Luigi Guelpa, ameweka wazi kuwa tayari Juventus wamekubaliana na Guardiola.

Guelpa amedai kuwa habari hizo ni za uhakika kwa kuwa amezipata kwa chanzo cha habari ambacho kilimpa taarifa juu ya Cristiano Ronaldo kutaka kuondoka Real Madrid na kujiunga na Juventus.

“Nimepata habari za uhakika kwamba Guardiola amefikia makubaliano na Juventus kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo kwa mkataba wa miaka minne ijayo, taarifa hiyo nimeipata kwa mtu ambaye aliniambia kwamba Ronaldo anakwenda kujiunga na Juventus,” alisema mwandishi huyo.

Guardiola aliyezaliwa January 18, 1971 ambaye mkataba wake unatarajia kumalizika mwishoni mwa msimu wa 2021, ameweka historia ya kutwaa Ligi Kuu nchini Hispania, Ujerumani na England,  pia ni miongoni mwa wachezaji bora katika nafasi ya kiungo  kutokea duniani katika miaka ya 1990's.