Rais awaonya wanaopuuza na kutoheshimu sheria


Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ameonya kuwa licha ya kuwapo kwa sheria tisa zinazohusiana na matumizi bora na endelevu ya ardhi, bado watu hawaziheshimu wala kuzifuata.

Akizungumza wakati akifungua semina kuhusu masuala ya ardhi na mali zisizorejesheka iliyofanyika mjini Unguja, alisema lengo la kuhakikisha ardhi inatumika vyema limeifanya serikali kutunga sheria tisa kuhusiana na matumizi bora na endelevu ya rasilimali hiyo.

Alizitaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni ya Matumizi ya Ardhi Na. 12 ya Mwaka 1992, Sheria ya Uhaulishaji wa Ardhi Na. 8 ya Mwaka 1994 na Sheria ya Mahakama ya Ardhi Na. 7 ya Mwaka 1994, ambayo ndiyo inayohusiana na uanzishwaji wa mahakama hiyo.

Dk. Shein alisema katika ziara yake aliyoifanya katika wilaya zote za Unguja na Pemba mwezi uliopita amefahamu mengi kuhusiana na kadhia ya kuvunjwa kwa sheria mbalimbali zinazohusiana na matumizi bora ya ardhi.

Alieleza kuwa kwa bahati mbaya wavunjaji wa sheria hizo ni viongozi na watendaji wa serikali na matukio mengine yanayofanywa na wananchi wa kawaida.

“Taarifa za wilaya zilizowasilishwa kwangu zote zimethibitisha kuendelea kuibuka kwa migogoro mipya ya ardhi katika wilaya iko ya uvamizi wa maeneo ya serikali, mingine ni baina ya wananchi na wawekezaji,” alisema Dk. Shein.

Aidha, alieleza kuwa jambo jingine ni kuwapo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira katika maeneo yanayochimbwa mchanga aliyoyatembelea ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa upungufu wa mchanga wenyewe.