Serikali yashauriwa kuandaa mpango wa haraka kunusuru Ziwa Manyara


Serikali yatakiwa kuandaa mpango Mkakati wa haraka wa kunusuru Ziwa Manyara ambalo liko hatarini kutoweka kutokana shughuli za kibadamu.

Ushauri huo umetolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Wakiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Manyara, Kamati hiyo imetembelea Ziwa Manyara na kujionea kupungua kwa kina cha maji kwa kiasi kikubwa kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kilimo kisicho endelevu hususan katika vyanzo vya maji kinachopelekea ziwa hilo kujaa tope pamoja na ongezeko la mimea vamizi.

Akizungungumza kwa niaba ya Kamati yake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Murad Sadick amesema ni wakati muafaka sasa jambo hili kupewe kipaumbele ili kunusuru hali ya sasa inayotishia uhai wa ziwa hilo.

“Sote tumejionea hali halisi, hali ni mbaya, mimi na Kamati yangu tunawajibu wa kuishauri Serikali, hatua za haraka na za maksudi kunusuru hali hii, hata kwa maziwa mengine pia kama Ziwa Jipe na Ziwa Chala. Endapo hatua za haraka hazitachukuliwa ndani ya miaka kumi ijayo Ziwa hili litatoweka. Ikumbukwe kuwa ziwa hili ni chanzo kikubwa cha kukuza pato la Taifa kupitia Utalii hapa nchini” Alisisitiza Mhe. Sadick.

Akiwasilisha hatua za zilizochukukuliwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuhusu kunusuru ziwa hilo Naibu Mkurugenzi Bw. William Mwakilime amesema kuwa Ofisi yake imechukua hatua za makusudi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa Umma juu ya namna bora ya kuwa na kilimo endelevu kinachozingatia matumizi bora ya ardhi na kujenga mabwawa maalumu kwa ajili ya kuchuja maji.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muugano na Mazingira Mheshimiwa January Makamba alieambatana na Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge katika ziara hiyo, amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha andiko jumuishi litakalogusa sekta zote kwa kuwa ni suala mtambuka na kuahidi kuwa Serikali inalipa uzito jambo hilo kwa mustakabali wa nchi na ustawi wa wananchi wake.