3/15/2019

Serikali yatoa hatimiliki za kimila 100 kwa wananchi


Serikali imetoa hatimiliki za kimila 100 kwa wananchi wa kijiji cha Mbondo wilayani Nachingwea ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa urasimishaji rasilimali ardhi vijijini  kwa lengo la kuwawezesha wananchi hao kiuchumi.


Hati hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Jason Rweikiza (Mb) wakati wa ziara ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo mkoani Lindi ikiwa ni pamoja na kujiridhisha namna Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) inavyotekeleza majukumu yake.

Rweikiza amesema hati hizo ni muhimu kwa wananchi hao kujiendeleza kiuchumi kwani zitawawezesha kuchukua mikopo kwenye taasisi za kifedha kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo ikiwemo zao la korosho ambalo ndio zao kuu la kibiashara mkoani Lindi.

Mhe. Rweikiza amewaasa wananchi waliopata hati hizo kuzitumia vizuri ili ziweze kuwanufaisha kiuchumi, na kuwahamasisha wale ambao hawaoni umuhimu wa kupata hati za kimila kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kupiga hatua kimaendeleo.

Ili kuwarahisishia wananchi wa kijiji cha Mbondo na vijiji jirani kupata hatimiliki za kimila, Mhe. Rweikiza ameiagiza MKURABITA kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa Masijala ya Ardhi kabla ya mwaka huu kuisha.

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amedhihirisha kwa vitendo kuwajali wanyonge hasa walioko maeneo ya vijijini kwa kuwapatia hatimiliki za kimila ili ziweze kuwasaidia kuondokana na umaskini.

Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, hati hizo za kimila zinatambuliwa na taasisi za kifedha nchini, hivyo zitawawezesha wananchi hao kupata mikopo kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa ametoa wito kwa taasisi za kifedha nchini, kuhakikisha zinatoa kipaumbele kwa wananchi wenye hati za kimila pindi wanapohitaji huduma ya mkopo.