Umuhimu wa chanjo katika afya zetu

Siku zote sisi wanadamu huwa tunaambizana kuwa, kinga ni bora kuliko tiba, tukiwa na maana kwamba, ni vyema mtu ukachukua tahadhari mapema kabla haujafikwa na jambo au tatizo fulani.

Vivyo hivyo katika chanjo, hii ni kinga ambayo hutolewa kwa binadamu na katika umri tofauti tofauti ili kuuwezesha mwili kutengeneza ulinzi asilia (antibodies) ambao utauwezesha mwili uwe na nguvu zaidi za kupambana na magonjwa au visababishi vya matatizo mbalimbali ya kiafya ambavyo siku zote vimekuwa ni sehemu ya maisha ya mwanadamu.

Mpenzi msomaji, ni vyema ukafahamu kuwa chanjo SIYO tiba, na siku zote hutolewa kwa watu ambao hawana ugonjwa au tatizo husika linaloendana na chanjo hiyo, mfano, kama mtoto anao ugonjwa wa surua, basi itabidi apate matibabu ya surua na siyo chanjo ya surua. (Ila kumbuka kuwa matatizo mengine ya kiafya kama vile kukohoa, kuharisha au mafua, havimzuii mtu kupata chanjo). 

Pengine utajihoji ni kwa nini inakuwa hivi?, hii ni kutokana na kwamba, chanjo siku zote dozi za dawa zake huwa ni kidogo ukilinganisha na dozi endapo hiyo dawa itatumika kutibu ugonjwa husika mfano surua au kifua kikuu, hivyo kwa kuwa dozi ni ndogo, basi haitakuwa rahisi kutibu mtu ambaye tayari anao ugonjwa.

Kitu kingine katika chanjo ni kwamba, baadhi ya chanjo huwa ni chembe chembe maalumu ambazo hufanana na aina ya ugonjwa ambao umekusudiwa kuzuiliwa au kukingwa, hivyo chembe chembe hizi huwa katika kiwango kidogo sana ambacho hakiwezi kukusababishia matatizo yoyote ya kiafya, ila mwili wako utaamshwa utengeneze kinga za kutosha ili endapo mazingira uliyopo yatakuwa na ugonjwa huo husika, wewe mwili wako utakuwa tayari kupambana ila chembe chembe hizi maalumu hazitaweza kukutibu endapo tayari unao ugonjwa husika.

Mambo ambayo huweza kujitokeza baada ya mtu kupata chanjo ni pamoja na hali ya joto la mwili kupanda au homa, ingawaje siyo lazima mtu apatwe na hali hiyo cha kufanya ni kutumia dawa za kushusha homa na baada ya muda mwili wako utarejea katika hali yake ya kawaida, hivyo endapo hali hiyo itajitokeza kwako usiwe na shaka.

Chanjo itakuwezesha kujikinga dhidi ya magonjwa, kukupunguzia gharama za matibabu na utapata muda ya kuendelea na shughuli zako za kila siku, kwani wewe au familia yako mtakuwa na afya bora.