Usalama waimarishwa Christchurch wakati shughuli zikianza tena


Usalama umeimarishwa katika mji wa Christchurch nchini New Zealand Jumatatu ya leo, wakati shule na biashara zikifungua milango kwa mara ya kwanza tangu shambulizi la kigaidi dhidi ya miskiti miwili katika mji huo, ambamo watu 50 waliuawa.

Mshukiwa wa shambulizi hilo, Brenton Tarrant ambaye anajinadi kuwa mfuasi sugu wa sera za kuwaenzi Wazungu anaendelea kushikiliwa rumande, wakati uchunguzi ukifanyika katika nchi kadhaa, na New Zealand ikiandaa kikao maalum cha baraza la mawaziri kujadili hatua za kuchukuliwa kuhusiana na shambulizi hilo.

Makaburi yamechimbwa tayari kwa mazishi ya baadhi ya wahanga wa shambulio hilo la kigaidi baadaye leo.

 Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern amezishinikiza kampuni za mitanado ya kijamii kutoa maelezo juu ya namna mshambuliaji alivyoweza kurusha moja kwa moja mitandaoni shambulizi lake kwa muda wa dakika 17, na vidio ya shambulizi hilo kuenea mitandaoni kwa masaa kadhaa. Amesema pia kuwa nchi yake itaimarisha sheria ya umiliki wa bunduki.