https://monetag.com/?ref_id=TTIb Wagonjwa watano wapandikizwa figo hospitali ya Benjamin Mkapa tangu kuanzishwa | Muungwana BLOG

Wagonjwa watano wapandikizwa figo hospitali ya Benjamin Mkapa tangu kuanzishwa


Hospitali ya Benjamin Mkapa imefanikiwa kupandikiza Figo jumla ya Wagonjwa watano tangu ilipoanza kufanya huduma hiyo kwa kushirikiana na Madaktari kutoka shirika la afya la Tokushukai lilopo nchi ya Japan.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za kibingwa za magonjwa ya Figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa Idadi ya wagonjwa waliokwishapandikizwa figo hapa nchini ni 43, ambapo 38 wamepatiwa huduma hiyo kwenye hospitali ya Taifa Muhimbili na wagonjwa watano(5) hospitali ya Benjamin Mkapa "Hivi navyoongea tayari mgonjwa mmoja amekwishapandikizwa figo na ameshatoka salama, yupo anaendelea kuangaliwa, lakini wana mpango wa kuwafanyia wengine wawili tutapokuwa tumekamilisha hili tutakuwa na wagonjwa saba ambao wamefanyiwa hospitali hii" alisema Dkt. Ndugulile.

Dkt. Ndugulile aliendelea kusema kuwa, Serikali imelenga kuhakikisha kwamba inawajengea uwezo Wataalamu wa ndani kufanya upasuaji wa kibingwa ili waweze kuwahudumia Watanzania bila msaada kutoka Wataalamu wa nje.

 "Lengo na kusudio ni kuhakikisha kwamba tunajenga uwezo wa ndani wa kuweza kufanya upasuaji huu" Alisema Dkt. Ndugulile

Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali imeokoa zaidi ya kiasi cha shilingi bilioni 4.2 ambacho kingetumika katika matibabu ya wagonjwa 80 mpaka 100 ambao wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu. “Wagonjwa waliokwishapandikizwa figo hapa nchini ni 42, kama tungewapeleka wagonjwa nje ya nchi ingegharimu serikali kiasi cha shilingi bilioni 4.2 kwa idadi hiyo ya wagonjwa. 80 mpaka 100, wakati huduma hii hapa nchini inagharimu kiasi cha shilingi milioni 21 kwa kila mgonjwa.” alisema Dkt. Ndugulile

Aidha, Dkt. Ndugulile amewashukuru Wataalamu kutoka shirika la Tokushukai kutoka nchi ya Japan kwa kujitoa na kuja kuwajengea uwezo Wataalamu wa ndani hali iliyosaidia kupunguza kiasi kikubwa cha fedha ambacho hutumika kwa ajili ya matibabu kwa wagonjwa wanaoenda kutibiwa nje.