Waziri ashtuka baadhi ya Watendaji wake kupandishana vyeo kiholela


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema ana taarifa za baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo kupandishana vyeo kiholela kutokana na kujuana.

Kutokana na changamoto hiyo, waziri huyo amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dorothy Mwanyika, kuhakikisha watendaji wa Wizara hiyo wanapewa nafasi za kuongoza kwa uwezo wao na si upendeleo kama ilivyokuwa awali.

Waziri Lukuvi aliagiza kufanyika kwa mchujo wa watendaji wa wizara hiyo kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakiipa sifa mbaya wizara kutokana na kujihusisha na rushwa na kuonea wananchi.

Lukuvi alifichua changamoto hiyo jana jijini Dodoma alipofungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo kilichojadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19 na mwelekeo wa bajeti ya mwaka huu wa fedha (2019/20).


Alisema kuna vijana wengi wenye uwezo, lakini wanaminywa na kunyimwa nafasi hizo kutokana na mafaili yao kuonekana "ni mepesi na hawana uzoefu kazini".


"Matokeo yake, wizara inakosa ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake kutokana kuwa na viongozi wasio na tija wala sifa ya kutekeleza majukumu husika. Siwezi kukubali mtu anasukumiwa jalada wakati mtu hana uwezo, halafu yeye anapitisha na kumpa mtu cheo," alisema.

Lukuvi aliagiza kuwa kufikia Julai 7, mwaka huu, watumishi wote kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa, wawe chini ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo.