Waziri Mbarawa atoa agizo EWURA


Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuwa na mfumo utakaotumika kupima gharama za maji kuendana na nishati inayotumika katika uzalishaji.

 Amesema hayo jijini Dodoma katika Wiki ya Maji, ambapo Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira  Tanga imepata tuzo kwa kuwa mamlaka bora katika huduma ya majisafi, wakati Mwanza imepata tuzo katika huduma ya uondoaji majitaka.

Prof. Mbarawa amesisitiza bei za maji zifanyiwe tathmini, pamoja na mengine, kwa kigezo cha nishati inayotumika kwa uzalishaji iwapo ni jua, umeme au huduma ya maji kutolewa kwa msesereko. Amesema imebainika gharama za maji maeneo ya vijijini ni kubwa kuliko mijini.

Ameitaka EWURA pamoja na kudhibiti inatakiwa iangalie namna bora ya kuikuza sekta ya maji, kwasababu  huduma  ya maji ikikua, mamlaka hiyo itafanya kazi zaidi kuwezesha wananchi kupata huduma bora. Pamoja na hilo, Waziri Prof. Mbarawa amesema mamlaka hiyo inatakiwa kuwa na programu ya kuwajengea uwezo Wahandisi na wataalam wa maji katika eneo la utawala na menejimenti ili watoe huduma vizuri zaidi kwa wananchi.

Pamoja na hilo, ameitaka mamlaka hiyo kufanya utafiti kujua umeme na dawa za kutibu maji kwa lita moja vinatumika kwa kiasi gani ili kuangalia namna bora ya kuagiza dawa za kutibu maji kwa pamoja ili  kupunguza gharama. Aidha, Waziri Prof. Mbarawa, pamoja na hilo amesema ni muhimu kuwa na mfumo wa kuonyesha hali halisi ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi kwa muda wowote.

Awali, akiongea kuhusu huduma za maji, Katibu Mkuu Wizara ya Maji Prof. Kitila Mkumbo amesema pamoja na mamlaka za maji kufanya biashara, uhalisia wa kinachofanyika ni huduma kwa wananchi hivyo taasisi nyingine zielewe na kuzingatia hilo.