https://monetag.com/?ref_id=TTIb Waziri Mkuu wa Pakistan awatahadharisha magaidi. | Muungwana BLOG

Waziri Mkuu wa Pakistan awatahadharisha magaidi.


Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan amesema kuwa hatoruhusu genge lolote la kigaidi kuendesha shughuli zake nchini humo na kusisitiza kuwa nchi hiyo sio makazi ya magaidi, amesema hayo mbele ya wafuasi wake kusini mwa Pakistan na kuongeza kuwa, serikali yake haitowaruhusu magaidi kutumia ardhi ya nchi hiyo kushambulia nchi jirani.

Matamshi hayo ya Waziri Mkuu wa Pakistan yamekuja siku chache tangu ulipopamba moto mzozo baina ya nchi hiyo na India kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyowalenga wanajeshi wa India.

Mzozo mpya katika uhusiano wa Pakistan na India ulizuka baada ya kundi la kigaidi linalojiita Jaish al Muhammad kushambulia wanajeshi wa India huko Kashmir tarehe 14 mwezi ulioisha wa Februari na kuua wanajeshi 44.

Jeshi la India lilituma ndege zake na kushambulia baadhi ya maeneo ndani ya ardhi ya Pakistan likidai kuwa ni maficho ya magaidi hao. Pakistan nayo ilijibu mashambulizi hayo ya India kwa kutungua ndege mbili za nchi hiyo na kumteka nyara rubani mmoja wa India ingawa baadaye ilimuachilia huru ili kuonesha nia yake njema.

Siku moja kabla ya kushambuliwa wanajeshi wa India, basi lililokuwa limebeba walinzi wa mpakani wa Iran lilishambuliwa huko Zahedan, makao makuu ya mkoa wa Sistan na Baluchistan wa Iran unaopakana na Pakistan na kusababisha maafisa 27 wa Iran kuuawa na wengine 13 kujeruhiwa.

Kundi la kigaidi la Jaish al Dhulm linaloendesha shughuli zake katika ardhi ya Pakistan lilijigamba kuhusika na shambulio hilo.