Albert Msando atoa ushauri kwa Wasanii nchini


Wakili wa wasanii Alberto Msando amewataka wasanii wote nchini kujitathimini upya katika mikataba au makubaliano wanayoingia na makampuni, mashirika, wamiliki wa filamu kwenye kazi zao.

Msando ameyasema hayo katika kongamano la waigizaji lililoandaliwa na bodi ya filamu (TFB) pamoja na Chama cha waigizaji (TDFAA)  lililofanyika ukumbi wa Suma JKT Mwenge jijini Dar es salaam, na kusema kuwa ni wakati wa Wasanii kujitathimini na kuingia makubaliano ya kikazi kwa njia ya maandishi ili kuepuka unyonywaji na utapeli kwenye malipo baada ya kazi na kabla ya kazi.

"Mikataba inasaidia wasanii kuwa na adabu na nidhamu ya kazi kutokana na kumtaka muda maalum kuwepo kwenye kazi na hata hivyo inamsaidia msanii kudai stahiki zake  haraka huku akiwa na vielelezo husika ," alisema Msando.

Msando amewataja baadhi ya wadau wakiwemo waandaaji wa filamu,watunzi wa filamu pamoja na watengenezaji wa matangazo ambao wanawatumia wasanii kwenye matangazo hayo, kuwa na leseni za kikazi ili kutambulika kisheria.

Halikadhalika amewatolea mfano wasanii kama Ambwene Yesya a.ka AY Khamisi Mwinjuma a.k.a MwanaFA,Wema Sepetu pamoja na Masanja Mkandamizaji ambao wameshapata matatizo kwenye kazi zao kutokana na mikataba wanayoingia na wakifika katika mikono sheria wanafanikiwa kupata haki zao ,Hivyo amewasihi wasanii kufika kwenye vyombo vya sheria au hata kusaini mikataba na kuhusisha Mawakili .

Pia ametoa rai kwa wasanii kujiandikisha kwenye vyama vya sanaa,bodi ya filamu pamoja baraza la sanaa ili kutambulika kama msanii mwenye kutambulika.