Askari FFU wajitolea damu kusaidia jamii


Askari polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoani Kagera wamejitolea kuchangia damu ili kukabiliana na upungufu wa damu unaoukabili mkoa huo na kutishia maisha ya makundi yanayohitaji kuongezewa damu wakiwamo wajawazito.

Askari hao wamejitolea damu kusaidia makundi hayo wakiwamo watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na majeruhi wa ajali.

Wakizungumza wakati wa zoezi hilo, baadhi ya askari waliozungumza na waandishi wa habari waliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kujitolea damu, ili kuokoa maisha ya Watanzania wenzao wanaohitaji kuongezewa damu.

Mmoja wa askari hao, Juma Ramadhan, alisema ameguswa na tatizo la watu wanaopoteza maisha kwa sababu ya kukosa damu, na kuwaomba askari wenzake kujitokeza kuchangia damu ili kunusuru maisha ya wananchi wenzao.

Askari mwingine, Slyvester Mazanza, alisema kuwa yeye kama askari anayelinda raia na mali zake hapendi kusikia raia apotee kwa kukosa damu wakati ana uwezo wa kujitolea damu.

“Kuna ndugu zetu kama wajawazito ambao wanapoteza damu nyingi wakati wa kujifungua na watoto, wanahitaji kuongezewa damu, sisi kama askari tumejisikia fahari kushiriki katika zoezi hili,” alisema.

Sajenti Charles Fabian alisema ni vema askari kuwa mfano kuchangia damu na kuwa wao wako tayari kuchangia muda wowote wanapohitajika kufanya hivyo, ili kuhakikisha afya za Watanzania ziko salama.