Bunge la Yemen lakutana kwa mara ya kwanza tangu 2015


Rais wa Yemen Abdu Rabbo Mansour Hadi amehudhuria kikao cha nadra cha bunge katika mji wa mashariki mwa Yemen. Kikao cha Baraza la Wawakilishi kilianza leo Jumamosi katika mji wa Sayoun kwa mara ya kwanza tangu kuzuka vita mnamo Machi 2015 kati ya wanajeshi wa serikali inayoungwa mkono na Saudi Arabia na waasi wa jamii ya Houthi, ambao wanadhibiti mji mkuu wa Sanaa.

Wabunge 130 wamehudhuria kikao hicho na kumchagua Sultan al-Borkani kuwa spika wa bunge. Bunge hilo lenye viti 301 lilichaguliwa kwa muhula wa miaka sita mnamo mwaka 2009 na limegawanyika kati ya wabunge wanaowaunga mkono waasi wa Houthi, upande wa serikali pamoja na wale wa kujitegemea.

Serikali ya Yemen imekuwa na makao yake mjini Aden tangu mwaka 2015, lakini Rais Hadi na viongozi wengine wa ngazi za juu wamekuwa wakiishi uhamishoni nchini Saudi Arabia