CUF wapania kuchukua ubunge wa Zitto Kigoma Mjini


Chama cha Wananchi (CUF) kimeomba wakazi wa Kigoma mjini kuunga mkono harakati za kisiasa za chama hicho ili kiibuke na ushindi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.

Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Kigoma Mjini, Yasini Mambobado amesema kuwa chama hicho kimejipanga kushinda viti vingi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu wa 2020 na kujitwalia jimbo hilo.

“Tumejipanga kushinda wenyeviti wa mitaa wengi mwaka huu na mwaka ujao kwenye Uchaguzi Mkuu tutashinda madiwani wengi na ubunge hapa Kigoma Mjini,” Mambobado amesema leo kwenye mkutano wa Asasi ya Meza Duara mjini humo.

“Nitoe wito kwa watu wanaotaka kugombea uenyeviti wa mitaa, udiwani na hata ubunge hapa Kigoma Mjini wasisite kufanya hivyo na chama pekee kitakachowafanya kushinda ni CUF,” aliongeza.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Meza Duara alihoji uhalisia wa kauli ya Mambobado; alihoji ni kwanini wanachama wa chama hicho wengi wamehamia ACT-Wazalendo kama kimezidi kuwa imara.

Mambobado alieleza kuwa chama hicho kimemaliza mgogoro na sasa kimewapata viongozi waadilifu ambao wameanza kukiimarisha Visiwani Zanzibar na baadaye watafanya hivyo upande wa bara ili kujihakikishia ushindi.