.

4/15/2019

Dkt. Kilahama atoa wito kwa Wasanii


Na.Ahmad Mmow, Kilwa Masoko

Wasanii wa muziki nchini wameaswa kuanza kuimba nyimbo zinazoharakisha na kuchochea maendeleo badala ya nyimbo za mapenzi pekee.

Wito huo umetolewa leo na mwenyekiti wa bodi ya shirika la kiraia la uendelezaji na usimamizi wa mpingo(MCDI),  Dkt Felician Kilahama kwenye hafla ya uzinduzi wa upandaji miti katika mkoa wa Lindi, iliyofanyika katika mamlaka ya mji mdogo wa Kilwa Masoko.

Dkt Kilahama aliyewahi kuwa mkurugenzi wa misitu na nyuki nchini, alisema wasanii, hasa wanamuziki hawanabudi kuimba nyimbo zenye ujumbe unachochea na kuharakisha shuguli za maendeleo na uchumi.  Badala ya zile zinazozungumzia mapenzi pekee.

Alisema vikundi vya sanaa vinanafasi kubwa ya kufikisha ujumbe kwa jamii.  Hivyo nivema vitumie nafasi hiyo kuimba nyimbo zinazochochea maendeleo na uchumi wa nchi. Ikiwemo kuitahadharisha jamii kuhusu madhara ya uharibifu wa mazingira na faida ya kuhifadhi.

"Tutapendana vipi na mapenzi hayo yatendekaje wakati nchi ikiwa jangwa?  Sio lengo langu kuzuia nyimbo za mapenzi, lakini siziimbwe nyimbo za mapenzi tu wakati kuna mambo muhimu yanahitaji kutangazwa," alisisitiza Dkt Kilahama.

Aidha mwenyekiti huyo wa bodi alitoa wito kwa wakala wa huduma za misitu nchini(TFS) kuendelea kutoa elimu kwa jamii. Huku akiwaasa pia wanahabari kusaidia kupaza sauti kuhusu utunzaji wa mazingira.