https://monetag.com/?ref_id=TTIb Hatua za kufuata wakati wa kuchagua mchumba | Muungwana BLOG

Hatua za kufuata wakati wa kuchagua mchumba

Ifuatayo ni njia ya kisaikolojia ambayo mwanamke anaweza kutumia kumpata mwanaume mwenye kumfaa bila kufanya naye mapenzi tena ni jibu sahihi la kuondokana na mchezo wa kubahatisha kwa wanaume wanaosaka wapenzi wa kweli na si taksi bubu ambazo mchana huweka namba za njano usiku nyeusi.

Kwanza, Ni mwanamke/mwanaume mwenyewe kujifahamu na kufahamu vigezo vya mpenzi anayemhitaji katika maisha yake. Ifahamike kuwa kila mwanaume ana wake na kila mwanamke anaye wake wa maisha pia. Hivyo asiyekufaa wewe anawafaa wengine, kinachotakiwa ni wewe kujitambua kwanza ili umtambue umtakaye.

Wanawake/wanaume wengi hawafahamu wanahitaji wapenzi wa aina gani, hivyo wanajikuta kama watu wanaoingia sokoni bila kujua wanataka kununua nini? Ndiyo maana wengi wameangukia kwa matapeli wa mapenzi, wakachezewa na kuumizwa moyo bure.

Pili, Ni kuketi chini na kuorodhesha vigezo stahili vya mwanaume/mwanamke unayemtaka. Baada ya hapo orodhesha tena kasoro za mwanaume/mwanamke unazoweza kuzivumilia na zile ambazo huwezi kuzivumilia kabisa. Hii inatokana na ukweli kwamba mwanadamu hajakamilika, ana upungufu wake.

Tatu, Anza kumsaka kwa kutumia milango ya fahamu. Cha kufanya hapa ni kuruhusu macho yawaone wanaume/wanawake na kuwatathmini kwa maumbile yao ya nje na kisha kupata majibu kutoka moyoni juu ya kuvutia kwao ambako hutambulika kwa moyo kurithika na mwili kusisimka.

Nne, Kuanzisha safari ya kuchunguza tabia za nje na za ndani kivitendo. Hapa suala la ukaribu baina ya mwanaume na mwanamke linahitajika. Msingi unaotajwa hapa ni kujenga mazoea ya kawaida yasiyokuwa na masuala ya kimapenzi na ngono. Kutambuana, dini, viwango vya elimu, kabila na makundi ya marafiki ni mambo ya kuzingatia.

Katika uchunguzi huu mwanamke/mwanaume anayetafuta mpenzi hana budi kupitia na kumlinganisha huyo aliyempata na vigezo alivyojiwekea. Zoezi hili liendane na kuweka alama ya pata kila anapobaini kuwa mwanaume/mwanamke anayemchunguza amepata moja ya vigezo vyake. Lakini pia aweke alama ya kosa kwa kila kasoro anayoivumilia na ile asiyoivumilia.

Tano, Ajipe muda wa kutosha kati ya miezi sita na mwaka kumchunguza huyo mwanaume, kisha aketi chini na aanze kujumlisha alama za vigezo alivyovijiwekea na jinsi mwanaume huyo alivyopata au kukosa.

Ikibainika mwanaume aliyechaguliwa amepata zaidi ya nusu ya alama ya vigezo vilivyowekwa, basi ujue kuwa anafaa. Kuhusu alama chache alizikosa anaweza kusaidia kuzikamilisha polepole wakati wa maisha ya ndoa.