Kenya yaanza kampeni ya kuwa mwanachama wa Baraza la Usalama la UN




Kenya imeanza kampeni ya kuwa mwanachama asiye wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Taarifa zinasema serikali ya Kenya inatazamiwa kuzindua rasmi kampeni yake hiyo mwezi Juni ambapo tayari imeshaanzisha mazungumzo na nchi za Umoja wa Afrika.

Katibu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya Macharia Kamau anasema kuingia kenya katika taasisi hiyo yenye nguvu zaidi katika Umoja wa Mataifa kutasaidia katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo endelevu, usalama wa kieneo na pia masuala ya mazingira na hasa mabadiliko ya tabianchi.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina wanachama watano wa kudumu ambao ni China, Russia, Uingereza, Ufaransa na Marekani na pia kuna wanachama 10 wasio wa kudumu ambao huchaguliwa kwa mzunguko kwa muhula wa miaka miwili. 

Kimsingi, wanachama watano wa kudumu wa Umoja wa Mataifa ndio ambao huchukua maamuzi muhimu kuhusu amani na usalama duniani na wanaweza kutumia kura ya turufu kupinga maamuzi muhimu. Kenya iliwahi kuwa mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama mwaka 1973 na 1997 na ilitumia fursa yake hiyo kutetea utatuzi wa amani wa migogoro na uhuru wa nchi ambazo zilikuwa zinapigania ukombozi.

Uanachama wa Kenya unatazamiwa kupigiwa kura katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York mwezi Septemba mwaka huu. 

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na harakati za kutaka kuwepo mabadiliko katika muundo wa Baraza la Usalama kwa kuongezwa wanachama wa kudumu wenye haki ya kura ya turufu. Nchi za Afrika zimekuwa zikipaza sauti  zikisema bara hilo linapaswa kuwa na kiti cha kudumu katika baraza hilo.