Kocha wa Yanga SC amalizana na wachezaji watatu


Baada ya kumwagiwa mamilioni ya usajili wa awali Kocha wa Yanga SC, Mwinyi Zahera amefanikiwa kumalizana na wachezaji watatu wa kimataifa kwa kuwapa mikataba ya awali.

Ijumaa iliyopita Kocha huyo alikabidhiwa zaidi ya milioni 80 na kamati maalum ya hamasa ya timu hiyo kwa ajili ya kwenda kuingia mikataba ya awali na wachezaji wawili, mmoja raia wa Ivory Coast na Mnyarwanda anayechezea ligi ya Kenya, lakini mbali na hivyo pia amefanikiwa kumsainisha mkataba wa awali mchezaji mwingine kutoka DR Congo.

Taarifa inaeleza kuwa Zahera atamaliza usajili wake wa kimataifa mapema kwa kuwa kati ya wachezaji wote aliokuwa akiwahitaji ameshaanza kumalizana nao kwa kuwapa mkataba wa awali na kwamba anashindwa kuwaweka wazi kwa kuhofia kuingiliwa usajili wake na timu zenye uwezo mkubwa.

“Kamati ya hamasa ya uchangiaji tayari imeshaanza kutekeleza majukumu yake kwa kocha kwa kumpatia kiasi cha awali alichoomba na kwamba wamemtaka aseme mapema pale anapomalizana na mchezaji ili na waweze kukusanya michango kwa malengo kwani mbali na kumtafutia fedha za usajili, pia wana jukumu la kukusanya fedha za kulipa mishahara ya wachezaji hao,” kilisema chanzo hicho.