Manyara yataka Mkoa uwe sehemu salama kwa wanawake na watoto


Na John Walter-Manyara

Mkoa wa Manyara umeanza kutekeleza kwa vitendo mpango wa kumaliza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto [MTAKUWA] uliozinduliwa na Naibu waziri wa afya.

Mkoa wa Manyara umeanza kwa  kuwawezesha wanakamati kwa kuwajengea uwezo katika mafunzo maalum ya namna ya kuweza kubaini vitendo vya kikatili na kuripoti.

Serikali imeandaa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kwa lengo la kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii ya kitanzania kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

 Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000); Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia (2005); Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008); Sheria ya Makosa ya Kujamiiana – SOSPA (1998).

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo,Katibu Tawala mkoa wa Manyara Missaile Raymond Musa ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoa hapa amesema ili kukomesha vitendo hivyo ni lazima kila mmoja ashiriki kwa nafasi yake.

“Ni lazima wadau wote waweke nguvu ya pamoja kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto,hivyo mafunzo haya mliyopata yawe chachu ya kuleta mabadiliko katika jamii yetu ili wanawake na watoto waishi salama”.

Mafunzo hayo yamefanyika Mjini Babati na kuwakutanisha wajumbe wa kamati hiyo ambao kwa pamoja watashiriki katika kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Manyara.

Naye Mratibu wa kutekeleza Mkakati huo wa  MTAKUWA Anna Fissoo amesema lengo lao ni kuhakikisha kuwa  mpaka ifikapo 2021-2022 mkoa wa Manyara iwe sehemu salama kuishi wanawake na watoto.

Kupitia mafunzo hayo,wajumbe wa kamati hiyo wamejifunza kuhusu dhana ya masuala ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto lakini pia wamejifunza maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Aidha, taarifa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) za mwaka 2017 zinaonesha kuwa wanawake na wasichana wapatao milioni 750 Duniani waliolewa wakiwa chini ya miaka 18.