https://monetag.com/?ref_id=TTIb Mbunge amuomba Rais Magufuli afanye Ziara Mkoani Manyara | Muungwana BLOG

Mbunge amuomba Rais Magufuli afanye Ziara Mkoani Manyara


Na John Walter-MANYARA

Mbunge wa Jimbo la Kiteto (CCM) mkoani Manyara Emmanuel Papian amemuomba Rais John Pombe Magufuli afanye ziara katika jimbo hilo ili kumalizike kwa mgogoro wa wakulima na wafugaji uliodumu kwa miaka mingi.

Akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye wiki ya Jumuiya ya wazazi wa Chama hicho katika Kata ya Kibaya wilaya ya Kiteto mbunge huyo ameeleza kuwa kutokana na migogoro hiyo ya Wakulima na wafugaji kuendelea kufukuta katika maeneo hayo umefika muda sasa Rais John Pombe Magufuli  kufika mwenyewe na kuangalia namna ya kuitatua Migogoro hiyo ili jamii hiyo iweze kuishi kwa amani na utulivu.

“Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli anahitajika Kiteto aje kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji”, alisema Papian.

Ikumbukwe kuwa Rais Magufuli aliunda kamati maalum ya jopo la mawaziri kwa lengo la kuwatembelea  na kuwasilikiza wananchi kwenye  maeneo yenye migogoro hapa nchini ikiongozwa na mwenyekiti wake waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeo ya Makazi Wiliam Lukuvi,na katika maeneo  waliyoyatembelea ni pamoja Simanjiro na Kiteto.

Waziri Lukuvi alisema baada ya kupokea mapendekezo ya namna ya kumaliza mgogoro huo kutoka pande zote watafikisha suala hilo kwa Rais Magufuli ili atoe maamuzi.

Mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti alisema baadhi ya wafugaji wa kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro na Irkushbor wilayani Kiteto wanafukuzwa mara kwa mara na wakanyang’anywa mifugo yao zaidi ya 600.

Naye Mbunge wa jimbo la Simanjiro, James Ole Millya ni wakati sahihi wa kuweka mpaka ili ijulikane mwisho wa wafugaji hao na hifadhi ya Taifa ya Tarangire na pori la akiba la Mkungunero, kuliko mpaka wao kusogezwa kila wakati.