Mwanafunzi Chuo Kikuu amchoma kisu aliyekuwa mpenzi wake


Mwanafunzi wa kike wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Pwani, Kaunti ya Kilifi nchini Kenya, amechomwa visu mara kadhaa na mwanafunzi mwenzake anayedaiwa kuwa alikuwa mpenzi wake.

Mwanafunzi huyo aliyejulikana kwa jina la Naomi Chepkemboi, alichomwa visu mara kadhaa kifuani na kisha kukimbizwa katika hospitali ya Kaunti ya Kilifi anakoendelea kupatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa Jeshi la polisi, mtuhumiwa ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta aliyetambulika kwa jina la Henry Kipkoech, ambaye alikuwa mpenzi wake anashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma ya kufanya shambulio hilo.

Ripoti ya awali ya Polisi imeeleza kuwa Henry alifika kwenye nyumba ya Naomi jana asubuhi akiwa na begi lenye visu vitatu. Aliingia ndani na kufunga mlango kisha kuanza kumshambulia msichana huyo ambaye alipiga kelele za kuomba msaada. Wanafunzi wenzake ndio waliofanikiwa kumuokoa.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa na kupelekwa kwenye kituo cha polisi cha Kilifi ambako anashikiliwa kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria, kwa mujibu wa Citizen.